Mkutano wa mwaka wa Jukwaa la Viongozi wa Elimu ya Sekondari

Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Elimu Zanzibar, Nd. Abdalla Mohamed Mussa amesema kuwa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imepanga mkakati wa kutatua kero zote zinazo kwamisha maendeleo ya wanafunzi nchini. Kauli hiyo ameitoa wakati akifunga mkutano wa mwaka wa jukwaa la viongozi wa Elimu ya Sekondari yaliyoshirikisha wadau wa Elimu wa Mkoa wa Mjini Magharibi katika ukumbi wa hoteli ya Ocean View Kilimani. Aidha, amesema kwamba wizara kupitia Taasisi ya Elimu ya Zanzibar inaendelea kuchukua juhudi na kuhakikisha masomo ya Sayansi yanaendelea kufanywa vizuri kwani katika mabadiliko ya mtaala wizara imejipanga kuhakikisha vitabu vyote vinavyotakiwa kuanzia kidato cha kwanza na kuendelea vinapatikana kwa wakati. “Tayari mipango ipo na utekelezaji wake unaendelea. Kwa sasa Taasisi ya Elimu inamashirikiano ya karibu sana kimuundo na utendaji na Taasisi ya elimu Tanzania ambapo ni jitihada za viongozi wetu kuhakikisha wanayafanyia kazi mambo yote yanayopelekea kuleta matokeo mazuri”. Pia, amesema jitihada hizo zikiendelezwa kwa pamoja itakuwa chachu na muarubaini wa kuhakikisha mafanikio ya elimu yanaendelea kukua. Aidha Ametumia fursa hiyo kuwaomba walimu wakuu, wenyeviti wa skuli na wazazi kuwaelisha wazee kuwa wastahamilivu katika kipindi hichi cha mpito cha utekelezaji wa mabadiliko ya mtaala. Naye Meneja Mwandamizi wa Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari Zanzibar kutoka Shirika la Good Neighbors, John Masenza, amesema maendeleo mazuri ya elimu ya watoto wa mkoa wa Mjini Magharibi yametokana na mashirikiano ya wizara pamoja na wadau wengine wa elimu ambpo yamesaidia kupatikana kwa mafanikio mbalimbali yanayopimika na yanayoonekana. Pia, ameendelea kusema mkoa wa Mjini Magharibi unaongoza katika kiwango cha ufaulu ukilinganisha na mikoa mengine ya Zanzibar licha ya kuwa na changamoto katika ufaulu kwa somo la Biology ambalo ni changamoto kwa wilaya zote Nae Mwenyekiti wa kikao kazi hicho, Said Hemed Nassor, amelipongeza shirika la Good Neighbors kupitia Koica kuandaa kikao kazi hicho na kuahidi kwamba yale yote waliyokubaliana katika kikao hicho watakwenda kuyafanyia kazi kwa vitendo ili kuongeza ufaulu zaidi wa wanafunzi.