Uzinduzi wa Mafunzo kwa Walimu - Mtaala Mpya
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Ali Abbdulgulam Hussein amesema kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu kwa jamii juu ya Mtaala Mpya wa elimu, ili waweze kuutambuwa vizuri. Ameeleza hayo alipokuwa akifunguwa mafunzo ya mtaala mpya kwa waalimu wa Maandalizi na Msingi, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Elimu Zanzibar, yaliyofanyika Kituo cha walimu (TC Dunga), wilaya ya Kati Unguja. Amesema kuwa mtaala huo mpya wa umahiri utawajenga watoto kusoma kwa kudadisi na kuelewa haraka mambo jambo amnalo ni tofauti na hapo zamani ambapo walikuwa wakisoma kwa nadharia. “Mafunzo haya muyape umuhimu kuliko chochote na mutowe mafunzo mazuri kwa watoto ili wawe na mafananikio mazuri na pia muwe mabalozi wazuri kuhusiana na mtaala huu ambao kutokana na upya wake utakuwa na changamoto”, alisema. Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu Zanzibar Nd. Abdalla Mohamed Mussa amesema uwepo wa mtaala huo mpya wa ujenzi wa umahiri kutaleta mabadiliko katika sekta ya elimu. Aidha amesema mafunzo ni ya awamu ya pili ambapo katika awamu ya kwanza walitoa mafunzo kwa walimu 6,557 wa maandalizi na msingi kwa skuli za serikali na binafsi na awamu hii ya pili watatoa kwa walimu 6,457 kwa skuli zote za Zanzibar.