Muendelezo wa Utoaji wa Mafunzo kwa Walimu

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu Zanzibar Nd.Abdalla Mohamed Mussa amewataka Walimu wa Skuli za Maandalizi kuacha tabia ya kufanya kazi kimazowea na badala yake kutumia mbinu sahihi za kufundishia ikiwemo kuwashirikisha wanafunzi. Ameyasema hayo wakati akitoa nasaha kwa walimu wa maandalizi wanao patiwa mafunzo ya mtaala mpya yanayoendela katika kituo cha Walimu Wingwi na Mitiulaya Mkoa wa Kaskazini Pemba, amesema ni vyema walimu kutumia vitabu vya ziada na kiada kama nyenzo za kufundishia na sio kutumia vitabu vya Wanafunzi pekee. Aidha ameeleza kuwa mafunzo ya Mtaala mpya yatawasaidia kufahamu mbinu bora za utekelezaji wa mtaala huo na kuchochea mabadiliko kupitia ubunifu na vitendo kama mtaala unavyohitaji. Kwa upande wake Mkuu wa divisheni ya Mafunzo kwa Walimu kutoka Taasisi ya Elimu ya Zanzibar Bi.Mwana Ali Abdallah amesema Serikali imetumia gharama kubwa kuwekeza katika ya sekta ya elimu hivyo amewataka walimu kuyapokea Mafunzo hayo na kuyafanyia kazi. Akitao neno la shukurani Mratibu wa kituo cha Walimu Wingwi Nd, Abdallah Muhammed Shehe ameipongeza Wizara ya Elimu kupitia Taasisi ya Elimu kwa Kuratibu mafunzo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa Lengo la kuimarisha mafanikio katika Sekta ya Elimu Nchini.