Mafunzo ya Mtaala mpya wa Umahiri ngazi ya Sekondari yameanza Kisiwani Pemba.

Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Elimu ya Zanzibar Nd. Abdalla Mohammed Mussa amewataka walimu kuwatayari kuufanyia kazi Mtaala mpya wa Sekondari ambao unakusudia Kuwawezesha wanafunzi kuwa na ujuzi na utambuzi wa fursa zilizomo kwenye jamii. Akifungua mafunzo ya siku nne kwa wakufunzi wa walimu (TOT) huko katika Kituo cha walimu Michakaini kisiwani Pemba amesema katika utekelezaji wa Mtaala huo ni lazima walimu kuwa na utayari kwani wao ndio watekelezaji wakubwa wa mtaala huo wanaotegemewa katika kuwaandaa wanafunzi darasani. Aidha amewataka Wakufunzi wa walimu wanaopatiwa mafunzo hayo kwenda kuwafahamisha walimu kuwa Mabadiliko ya Mtaala ni jambo la kawaida kulingana na mahitaji ya jamii husika pamoja na Mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Amesema Mafunzo hayo yatawasaidia walimu katika kuutumia Mtaala mpya wa umahiri kwa Ngazi ya Sekondari. Akiwasilisha Mada ya Utelezaji wa Mtaala Ulioboreshwa kwa ngazi ya Sekondari Muwezeshaji Kutoka Taasisisi ya Elimu Tanzania Hwago Hassan Hwago amesema Elimu ya Sekondari sasa itakua na mikondo miwili ambayo ni mikondo wa Jumla na Mkondo wa Amali. Ameeleza kuwa Mtaala mpya wa Sekondari umetoa fursa kwa wanafunzi kujifunza Elimu ya Amali ili kuwawezesha wanafunzi hao kujiajiri wanapomaliza masomo yao.