Waziri Lela kuzindua Mtaala mpya wa Sekondari
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Muhammed Mussa amewataka walimu wa Sekondari Kisiwani Pemba kuyafanyia kazi mafunzo ya Mtaala Mpya wa Sekondari yanayotolewa na Taasisi ya Elimu ya Zanzibar kwa Kushirikiana na Taasisi ya Elimu ya Tanzania ili kuleta mabadiliko chanya kwa wanafunzi. Waziri Lela ameyasema hayo leo alipokuwa akizunguma na walimu, wanafunzi, Maafisa elimu na Maafisa wa Wizara ya Elimu katika Uzinduzi wa Mafunzo ya Mtaala Mpya wa Sekondari kwa Walimu wa Kidato cha Kwanza huko Skuli ya Utaani Wete Pemba. Amesema kuwa matarajio ya Wizara ya Elimu na Serikali ni kuona utekelezaji wa Mtaala huo unaanza kwa vitendo kwani Mtaala huo ndio ukombozi wa vijana wa kizanzibari. Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Nd. Khamis Abdullah Said amesema pamoja na mafunzo hayo serikali Kupitia Wizara ya Elimu itaendelea kutoa mafunzo kwa Walimu na haitaacha kuwafuatilia walimu kuona namna gani wanautekeleza kwa vitendo Mtaala huo. Amesema Serikali itaendelea kutimiza wajibu wake kwa walimu ikiwemo kuweka mipango mizuri ikiwemo sera na miundombinu rafiki akiahidi kuwa wizara itaendelea kuwa mtetezi wa maslahi ya walimu serikalini. Mapema Mkuregenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu Zanzibar Nd. Abdalla Mohamed Mussa ameahidi kuwa Taasisi hiyo itaendelea kutoa Mafunzo kwa Walimu kila itakapo hitajika ili kuhakikisha walimu wanaufahamu vyema Mtaala mpya wa Sekondari.