Uzinduzi wa programu 10 za Redio za kujifunza lugha ya Kiingereza
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imesema itaendela kufanya kazi kwa karibu na taasisi ya Zanzibar Milele Foundation kwa lengo la kuengeza nguvu na kuleta mabadiliko katika sekta ya Elimu nchini. Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu Zanzibar, Abdallah Muhammed Mussa, aliyasema hayo wakati akizundua programu 10 za redio za kujifunza lugha ya Kiingereza zilizotaarishwa na Milele Foundation kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu Zanzibar, hafla iliyofanyika Michenzani Mall mjini Unguja. Amesema, utekelezaji wa Mtaala wa Elimu sio jukumu la Serikali peke yake, bali taasisi mbali mbali zinapaswa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa suala hilo. Aidha amefahamisha kuwa matumizi ya lugha ni muhimu katika maendeleo ya nchi hivyo amewataka wazazi na walezi kushajihisha watoto wao kutumia lugha zote zinazofundishwa skuli ili waweze kuzifikia fursa zinazotokea katika nchi mbalimbali duniani Sambamba na hayo ameipongeza taasisi ya Milele Zanzibar Foundation kwa kuandaa programu ya vipindi vya elimu vitakavyorushwa kupitia Televisheni na redio mbali mbali ili kuongeza uelewq kwa wanafunzi wa mjini na vijijini. Kaimu Mkuu wa Miradi Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation, Ali Bakari Amani, amesema elimu inayotolewa inatoa uthubutu kwa watoto na kuwapa hamasa ya kufanya vizuri kwenye masomo yao. Nae meneja wa Miradi wa taasisi ya Milele Zanzibar Foundation, Eshe Haji Ramadhan, amesema lengo la kuanziasha mradi huo ni kuhakikisha watoto wanajua kusoma na kuandika lugha ya Kiingereza vizuri zaidi Amesema programu hiyo inahusisha wanafunzi wa skuli za Unguja na Pemba ambapo wanafunzi wanaoishiriki ni kuanzia skuli za msingi hadi sekondari, na elimu hiyo itatolewa kupitia Kwarara Media na redio nyengine za kijamii.