TEZ yafanya Mkutano na Walimu wakuu wa Skuli za Sekondari Pemba

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu ya Zanzibar Nd. Abdalla M. Mussa amewataka walimu wakuu wa skuli za Sekondari kisiwani Pemba kujiandaa na mapokezi ya Mtaala mpya wa Sekondari ambao utaanza kutumika hivi karibuni kwa Skuli zote nchini. Akizungumza katika Mkutano maalumu na walimu wakuu wa Skuli za sekondari Mkoa wa Kaskazini na Kusini Pemba huko katika Kituo cha Walimu Mitiulaya na Skuli ya Sekondari Madungu Amesema, Taasisi ya Elimu ya Zanzibar imeshaanza kuandaa Mchakato wa kutoa Mafunzo kwa Walimu wa skuli za Sekondari ambayo yatahusisha walimu wote wa skuli za serikali na binafsi. Amesema Mtaala mpya wa sekondari utawawezesha wanafunzi kujitegemea na kuweza kujiajiri wanapomaliza masomo ambapo mfumo wa Elimu ya Sekondari utakuwa na mikondo miwili ambayo ni Mkondo wa Amali na Mkondo wa Masomo ya kawaida. Ameelza kuwa katika mtaala huo kutakuwa na masomo mapya ambayo ni Pamoja na somo la Historia ya Tanzania na somo la Business study. Sambamba na hayo amewasisitiza walimu kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha wanatoa Takwimu sahihi za Walimu wanaohitaji kupatiwa mafunzo ili kila Mwalimu apate fursa ya Mafunzo hayo. Nao walimu wakuu wa skuli za sekondari Wameishukuru Taasisi ya Elimu ya Zanzibar kwa kuwapatia Tarifa muhimu kuhusu mtaala mpya kila inapohitajika na kushauri kupatiwa Mihutasari na vitabu kwa wakati.