Mjumbe wa Sekretarieti ya GPE Lucinda Ramos ametembelea TEZ
Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imefanya kazi kubwa katika eneo la uandaaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia vikiwemo Vitabu vya watoto wenye Mahitaji Maalumu ya kielimu nchini. Hayo ameyasema Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu ya Zanzibar Nd. Abdalla Mohamed Mussa wakati akizungumza na ugeni kutoka Mfuko wa Kusaidia Maendeleo ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education GPE) ambao umefika ofisi za Taasisi hiyo Mazizini kwa lengo la kubadilishana mawazo juu ya namna bora ya kuimarisha upatikanajinwa vifaa vya kufundishia na kujifunzia kufuatia mabadiliko ya Mtaala yanayoendelea, pia ugeni huo ulipata fursa ya kutembelea Skuli ya Kisiwandui ambayo inafundisha wanafunzi wenye Mahitaji Maalumu ya Kielimu. Amesema GPE imeisaidia Serikali kupitia Wizara ya Elimu juu ya upatikanaji wa vitabu ambavyo tayari vinatumika katika skuli mbalimbali nchini. Mjumbe wa Sekretarieti ya GPE Lucinda Ramos amesema Lengo la ziara hiyo ni kufanya ufuatiliaji wa miradi waliofadhili GPE katika Wizara ya Elimu ikiwemo Vitabu vinavyotumiwa na wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambapo amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kupitia Taasisi ya Elimu ya Zanzibar na kuahidi kuwa wataendelea kutoa ushirikiano katika maeneo hayo. Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Kiswiandui Nd. Ali Abdallah Mahmoud amesema ujio wa wageni mbalimbali kutembelea skuli hiyo unawapa moyo wanafunzi wenye Mahitaji Maalumu ya kielimu na amepongeza wizara kwa kuwekwa Utaratibu mzuri na kuandaa mazingira mazuri ya kujifunzia kwa wanafunzi.